Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
SIKU TATU ZA KUPIGA MSASA VIJANA DODOMA KUONGEZA T...

SIKU TATU ZA KUPIGA MSASA VIJANA DODOMA KUONGEZA TIJA YA MIKOPO

21 May, 2026
SIKU TATU ZA KUPIGA MSASA VIJANA DODOMA KUONGEZA TIJA YA MIKOPO

Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana kwa kushirikiana na Restless Development leo Mei 21, 2026 imehitimisha siku tatu za kutoa elimu ya fedha, biashara, na matumizi sahihi ya mikopo kwa vijana wa Mkoa wa Dodoma waliochaguliwa kwenye orodha ya kwanza ya wanufaika.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo kwenye ukumbi wa Restless Develeoment, Dodoma, Afisa Biashara, Ofisi ya Rais, Bw. Rashid Luhuiy amewapongeza washiriki wa mafunzo hayo kwa kuwa na miradi bunifu itakayowasaidia kukuza kipato chao, kutoa ajira kwa vijana wengine na kuchangia pato la taifa.

Pamoja na hayo amewataka washiriki hao kutumia kikamilifu elimu waliyoipata ikiwa ni pamoja na kujikita katika kutekeleza na kukuza miradi waliyoombea mikopo ili waweze kufikia malengo yanayotarajiwa ya kuwezesha vijana kukua kiuchumi.

“Ni muhimu kila kijana aliyenufaika na haya mafunzo afuate yote ambayo ameelekezwa ili kuweza kufikia kile ambacho serikali inakusudia kupitia mikopo ya vijana.”

Lucas Sangula ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo amesema kuwa moja ya jambo muhimu alilojifunza ni namna bora ya kuandika mpango wa biashara ili kuwa na muongozo sahihi wa usimamizi wa fedha na uendeshaji wa mradi wake.

Vilevile, Faith Maleke amesema kuwa mafunzo aliyopata yamemjengea uelewa kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara yake ili aweze kunufaika na fursa mbalimbali zikiwemo tenda za serikali.

Kwa upande wake Ally Saad, ambaye ni Mwezeshaji wa Mafunzo hayo kutoka Restless Development

ameishukuru Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana kwa kuwapa dhamana ya kutoa mafunzo hayo wezeshi kwa vijana, ili waweze kutumia mikopo wwanayopewa kufikia malengo yao na kuleta mabadiliko katika jamii.