Serikali imekabidhi pikipiki 22 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 87 kwa vikundi viwili vya vijana katika Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Mikopo ya shilingi bilioni 200 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana inayolenga kuwawezesha vijana kiuchumi.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amesema mpango huo unadhihirisha dhamira ya Serikali ya kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea kupitia mikopo isiyo na riba, ili kuimarisha ajira, kuongeza kipato na kuchochea ukuaji wa uchumi.
“Serikali itaendelea kutengeneza mazingira ya kuwafanya vijana wa nchi hii, wanapohitaji mitaji, wanapohitaji mazingira mazuri ya biashara, wasikwame katika maeneo yao,” ameongeza Mhe. Nanauka.
Amesema Kikundi cha Muungano, chenye wanufaika sita, kimepatiwa mkopo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 21 kwa ajili ya ununuzi wa pikipiki, huku Kikundi cha Safari na Usalama Bodaboda Njisi, chenye wanufaika 16, kikinufaika na mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 65.

Mhe. Nanauka amewataka wanufaika kutumia fursa hiyo kwa uwajibikaji, kusimamia kwa umakini mali walizokabidhiwa na kuhakikisha mikopo hiyo inakuwa chachu ya kuinua maisha yao na kuchangia maendeleo ya jamii.
Amesema Serikali itaendelea kubuni na kuimarisha programu zinazowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na ujasiriamali, huku akisisitiza kuwa nidhamu ya matumizi na urejeshaji wa mikopo ni msingi wa kuwafikia vijana wengi zaidi nchini.
“Ninaishukuru Serikali yetu kwa kutujali vijana na kutuwezesha kujiajiri na kujiletea maendeleo. Pikipiki tulizopewa leo zitatuinua kiuchumi na kutuwezesha kuanzisha miradi mingine itakayotusaidia kuongeza kipato na kuleta tija kwa jamii, ikiwemo kutengeneza ajira kwa vijana wengi zaidi.” Amesema mmoja wa wanaufaika wa mikopo hiyo.
Programu ya Mikopo ya shilingi bilioni 200 ni miongoni mwa mikakati ya Serikali ya kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa vijana, kukuza ajira na kuimarisha uchumi wa taifa kupitia uwekezaji katika shughuli za uzalishaji na biashara.
- "Huduma bora: Mafunzo ya NeST Morogoro yaiweka Ofisi ya...
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, ak...
- Makundi maalumu ikiwemo Vijana waaswa kujiunga NeST kupata fursa ya 30% ya Zab...
- Huduma bora kwa watanzania, NeST kutoa fursa kwa wazabuni wa...
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, am...