Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
MAPINDUZI YA KIDIJITALI: KULETA TIJA NA UWAZI KWEN...

MAPINDUZI YA KIDIJITALI: KULETA TIJA NA UWAZI KWENYE UNUNUZI KUPITIA NEST.

15 Jul, 2026
MAPINDUZI YA KIDIJITALI: KULETA TIJA NA UWAZI KWENYE UNUNUZI KUPITIA NEST.

-    Huduma bora kwa watanzania, NeST kutoa fursa kwa wazabuni wa ndani.
-    Makundi maalumu ikiwemo Vijana waaswa kujiunga NeST kupata fursa ya Asilimia 30.

KATIKA juhudi za kuboresha uwazi na ufanisi wa ununuzi wa umma, Maafisa mbalimbali wa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana wanaendelea kunolewa na mafunzo maalum ya vitendo kuhusu Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma, unaojulikana kama NeST (National e-Procurement System of Tanzania), ambayo yanafanyika leo tarehe 14 Julai 2026 mkoani Morogoro.

Akizungumza na washiriki wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bi. Edith Semtengu akimwakilisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, amesema mapinduzi ya kidijitali katika mfumo wa ununuzi wa umma (e-Procurement) kupitia NEST (National e-Procurement System of Tanzania) siyo tu uboreshaji wa kiufundi, bali ni uti wa mgongo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. 

Pamoja na msisitizo huo, amewasihi washiriki kutumia fursa hiyo kuendelea kuhudumia watanzania kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma. Ili kutimiza lengo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Pia amesisitiza makundi maalumu ikiwemo vijana kutumia fursa ya asilimia 30 katika mfumo wa NeST ili kujikwamua kiuchumi.

Mkufunzi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Wilson Samwel amesema mada zitakazofundishwa ni Usajili wa Taasisi na Wazabuni, Uandaaji na Uwasilishaji wa Zabuni, Tathmini na Utoaji wa Mikataba na Faida za Kutumia Mfumo wa NeST. Akasema kupitia mafunzo haya, washiriki wanakumbushwa faida mbalimbali za kimkakati zinazotokana na matumizi ya mfumo huu, ikiwemo Kuongeza Uwazi na Uwajibikaji, Kuokoa Muda na Rasilimali na Ushindani Huru na Haki.

Aidha Kaimu Mkurugenzi, Kitengo cha Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi, Bw. Hamisi Ally akiwakilisha washiriki takribani 35, amesema kukamilika kwa mafunzo haya kunatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa kiutendaji katika taasisi. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inahakikisha kuwa fedha za umma zinatumika kwa uhalali, ubora wa matokeo na thamani halisi ya fedha (Value for Money) inapatikana katika ununuzi wa umma.