Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
SERIKALI KUIMARISHA AFYA YA AKILI KWA VIJANA

SERIKALI KUIMARISHA AFYA YA AKILI KWA VIJANA

08 Jul, 2026
SERIKALI KUIMARISHA AFYA YA AKILI KWA VIJANA

“Tunataka kijana apate msaada mapema, karibu na mazingira yake, kwa namna inayoheshimu utu na usiri wake.”

Hayo yamesemwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Dkt. Kedmon Mapana, wakati akifungua kikao cha wataalamu cha kujadili andiko dhana la uanzishwaji wa Programu ya Huduma ya Msaada wa Kisaikolojia na Afya ya Akili kwa Vijana ambacho kimefanyika  Julai 8, 2026, katika Hoteli ya Kibo Peak Mkoani Morogoro.

Dkt. Mapana amesema kuwa uanzishwaji wa programu hiyo ni muendelezo wa jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweka mkazo katika ustawi, ulinzi, makuzi na maendeleo jumuishi ya vijana kwa kuzingatia kuwa Kundi hilo ndio nguvu kazi ya taifa.

"Vijana ni kundi kubwa, ni nguvu kazi ya Taifa, ni wabunifu, ni wazalishaji na msingi muhimu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi yetu," amesema, akisisitiza kuwa ni muhimu kuendelea kujenga mifumo madhubuti inayogusa ustawi wa vijana, ikiwemo huduma za msaada wa kisaikolojia na afya ya akili.

Ameongeza kuwa huduma za msaada wa kisaikolojia ni sehemu muhimu ya kuwawezesha vijana kukabiliana na changamoto za maisha kwa kuwa zinajumuisha kusikilizwa, ushauri, unasihi, mwongozo, msaada wa awali, rufaa na ufuatiliaji pale inapohitajika.

"Afya ya akili inaonesha ustawi wa kijana na msaada wa kisaikolojia ni mojawapo ya njia ya kumsaidia kijana kurejea katika hali hiyo anapokutana na changamoto.”

Aidha, amesema kuwa kuwa mpango unaoandaliwa unapaswa kuzingatia ushirikiano wa sekta zote zinazogusa ustawi wa vijana ili kuhakikisha huduma za msaada wa kisaikolojia na afya ya akili zinawafikia vijana kwa ufanisi na kukidhi mahitaji yao.

Dkt. Mapana amesisitiza kuwa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana itaendelea kushirikiana na wizara za kisekta, taasisi za elimu ya juu, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wengine ili kujenga mfumo endelevu wa huduma za afya ya akili unaowafikia vijana nchini.