Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
RASIMU YA PROGRAMU YA MSAADA WA KISAIKOLOJIA KWA V...

RASIMU YA PROGRAMU YA MSAADA WA KISAIKOLOJIA KWA VIJANA YAKAMILIKA

12 Jul, 2026
RASIMU YA PROGRAMU YA MSAADA WA KISAIKOLOJIA KWA VIJANA YAKAMILIKA

Serikali imekamilisha rasimu ya kwanza ya andiko dhana la Programu ya Huduma ya Msaada wa Kisaikolojia na Afya ya Akili kwa Vijana, hatua inayotarajiwa kuweka mfumo wa pamoja wa kuratibu utoaji wa huduma hizo na kuboresha upatikanaji wake kwa vijana nchini.

Rasimu hiyo imekamilika baada ya kikao cha siku tatu kilichowakutanisha wataalamu kutoka Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, wizara za kisekta, sekta binafsi na asasi za kiraia, ambapo wamejadili hali ya huduma za afya ya akili kwa vijana, changamoto zilizopo na mapendekezo ya namna bora ya kujenga huduma hizo ili ziendane na mahitaji ya makundi yote ya vijana nchini.

Mwezeshaji katika kikao hicho, Dkt. Lucas Kitula, amesema kuanzishwa kwa programu hiyo kutasaidia vijana kukabiliana na changamoto za afya ya akili na za maisha kwa ujumla, hivyo kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya Taifa. Hata hivyo, amesema kuwa  ubora wa huduma hizo unategemea ushiriki wa wadau katika kutoa maoni yatakayosaidia kuandaa programu zenye mahitaji halisi ya vijana.

"Tunachokifanya sasa ni kujenga mfumo utakaowawezesha vijana kupata huduma stahiki za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kwa urahisi zaidi. Tunawaomba wadau kutoa ushirikiano pale watakapohitajika ili tupate programu inayoakisi mahitaji halisi ya vijana," amesema Dkt. Kitula.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii, Lilian Msuha amesema kuwa kuanzishwa kwa Programu ya Huduma ya Msaada wa Kisaikolojia na Afya ya Akili kwa Vijana kutaimarisha uratibu wa utoaji wa huduma hizo kitaifa na kuhakikisha zinawafikia vijana kwa kuzingatia mahitaji yao.

Akihitimisha kikao hicho, Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi na Makuzi ya Vijana, Godfrey Massawe, amewapongeza wataalamu walioshiriki katika kikao hicho kwa kukamilisha rasimu ya kwanza ya andiko hilo kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana Dkt. Kedmon Mapana, wakati wa ufunguzi wa kikao.

Pia, ametoa wito kwa wataalamu hao kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana ili kuhakikisha mchakato wa kuanzisha programu hiyo unafanikiwa, hususan baada ya kukamilika kwa zoezi la kukusanya maoni kutoka kwa vijana na wadau wa maendeleo ya vijana yatakayotumika kuboresha andiko la mwisho la kuanzisha programu hiyo.