Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
PROGRAMU YA BILIONI 200 YAZINDULIWA ARUSHA, VIKUND...

PROGRAMU YA BILIONI 200 YAZINDULIWA ARUSHA, VIKUNDI VITATU VYANUFAIKA NA MILIONI 730

09 Jul, 2026
PROGRAMU YA BILIONI 200 YAZINDULIWA ARUSHA, VIKUNDI VITATU VYANUFAIKA NA MILIONI 730

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuweka mazingira wezeshi yanayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali kupitia Programu ya Mikopo ya Shilingi Bilioni 200 chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa utoaji wa mikopo hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Nanauka amesema mpango huo unalenga kuwawezesha vijana wenye miradi yenye tija kupata mtaji utakaowaongezea uwezo wa kuzalisha, kupanua biashara zao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa pamoja na kuongeza ajira kwa vijana wengine.

Katika uzinduzi huo, vikundi vitatu vya vijana kutoka Mkoa wa Arusha vimekabidhiwa mikopo yenye thamani ya jumla ya Shilingi Milioni 730 kupitia Programu ya Shilingi Bilioni 200 chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. 

Waziri Nanauka amesema mikopo hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuwawezesha vijana kuanzisha na kukuza miradi yenye tija, kuongeza thamani ya bidhaa na huduma, pamoja na kuchochea maendeleo ya uchumi katika ngazi ya jamii na Taifa.

Aidha, Mhe. Nanauka amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa, kuisimamia kwa uadilifu na kuhakikisha inazalisha matokeo yaliyokusudiwa ili kunufaisha vijana wengi zaidi kupitia mfuko huo. Pia amewahimiza vijana wengine kujitokeza kutumia fursa zinazotolewa na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana ili kujenga uchumi wao na kuchangia maendeleo ya Taifa.