Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo, ameupongeza Umoja wa Wabunge Vijana Tanzania (TYPC) kwa juhudi zake za kuimarisha ushirikiano na kujenga uwezo wa viongozi vijana nchini.
Prof. Mkumbo ametoa pongezi hizo Juni 16, 2026, wakati akifunga rasmi mafunzo ya Umoja wa Wabunge Vijana Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa Bunge, Dodoma.

Katika hotuba yake, Mhe. Prof. Mkumbo amewahimiza wabunge vijana kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao ya uwakilishi, huku wakitanguliza mbele maslahi ya Taifa na kuweka kando tofauti za kisiasa au mitazamo binafsi.
Amesema vijana wana nafasi muhimu katika kuimarisha maendeleo ya Taifa na kwamba wanapaswa kutumia nafasi zao za uongozi kuhamasisha uwajibikaji, ubunifu na ushiriki wa vijana katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa viongozi vijana kuendelea kujifunza, kujenga uwezo wao wa uongozi na kushiriki kikamilifu katika mijadala yenye tija kwa maendeleo ya Tanzania, akieleza kuwa nguvu ya umoja ndiyo msingi wa kufanikisha malengo ya maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, amewashukuru wabunge vijana kwa ushirikiano wao na mwitikio mkubwa katika mafunzo hayo, akieleza kuwa ushiriki wao ni ishara ya dhamira ya dhati ya vijana katika kuchangia maendeleo ya Taifa. Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi vijana katika kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo na maamuzi ya kitaifa.
Aidha, Mhe. Nanauka amemshukuru Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kufunga mafunzo hayo, akibainisha kuwa uzoefu, maarifa na ushauri alioutoa kwa wabunge vijana utakuwa chachu ya kuimarisha uongozi wenye maono, uzalendo na uwajibikaji kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wabunge vijana katika masuala ya uongozi, utungaji wa sera, ushiriki wa vijana katika maendeleo ya Taifa pamoja na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa viongozi vijana nchini.
- "Huduma bora: Mafunzo ya NeST Morogoro yaiweka Ofisi ya...
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, ak...
- Makundi maalumu ikiwemo Vijana waaswa kujiunga NeST kupata fursa ya 30% ya Zab...
- Huduma bora kwa watanzania, NeST kutoa fursa kwa wazabuni wa...
Serikali imekabidhi pikipiki 22 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 87 kw...