Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
NANAUKA AWAHAMASISHA VIJANA KUTUMIA UBUNIFU KAMA C...

NANAUKA AWAHAMASISHA VIJANA KUTUMIA UBUNIFU KAMA CHACHU YA MAENDELEO, AMPONGEZA MHE. MAJALIWA KWA KUENDELEA KUSAPOTI AJENDA YA VIJANA

19 Jun, 2026
NANAUKA AWAHAMASISHA VIJANA KUTUMIA UBUNIFU KAMA CHACHU YA MAENDELEO, AMPONGEZA MHE. MAJALIWA KWA KUENDELEA KUSAPOTI AJENDA YA VIJANA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, amewataka vijana nchini kuendelea kutumia ubunifu, maarifa na vipaji walivyonavyo kama nyenzo muhimu ya kujiletea maendeleo binafsi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mhe. Nanauka ameyasema hayo leo Juni 19, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na mamia ya vijana waliohudhuria Tamasha la Tanzania ya Thamani kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mshauri wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Kassim Majaliwa.

Amesema tamasha hilo ni jukwaa muhimu linalowawezesha vijana kuonesha bunifu zao, kuunganisha mitandao ya kibiashara, kujifunza kutoka kwa wadau mbalimbali na kutambua fursa zilizopo katika sekta tofauti za maendeleo.

“Mhe. Nanauka amewapongeza waandaaji wa Tamasha la Tanzania ya Thamani kwa kuandaa tukio lenye manufaa makubwa kwa vijana, akieleza kuwa juhudi hizo zinaunga mkono dhamira ya Serikali ya kuwawezesha vijana kiuchumi na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa,” alisema.

Aidha, amewahimiza vijana kutumia fursa zinazotolewa kupitia majukwaa mbalimbali ya ubunifu na ujasiriamali kwa kuzingatia nidhamu, ubunifu na uzalendo ili kujenga mustakabali bora kwao na kwa Taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Mhe. Nanauka amemshukuru Mshauri wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Kassim Majaliwa, kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi wa tamasha hilo na kwa kuendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuunga mkono ajenda za maendeleo ya vijana nchini.

Tamasha la Tanzania ya Thamani limewakutanisha vijana wabunifu, wajasiriamali, wasanii na wadau wa maendeleo kutoka sehemu mbalimbali za nchi kwa lengo la kukuza ubunifu, uzalendo, ujasiriamali na fursa za kiuchumi kwa vijana wa Tanzania.