Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
NANAUKA AMPONGEZA ESAU NG'UMBI KWA KUTWAA TUZO YA...

NANAUKA AMPONGEZA ESAU NG'UMBI KWA KUTWAA TUZO YA UMAHIRI WA UANDISHI WA HABARI

19 Jun, 2026
NANAUKA AMPONGEZA ESAU NG'UMBI KWA KUTWAA TUZO YA UMAHIRI WA UANDISHI WA HABARI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, amempokea na kumpongeza mwandishi wa habari kijana Esau Ezra Ng'umbi kufuatia mafanikio yake ya kutunukiwa Tuzo ya Umahiri wa Uandishi wa Habari (Excellence in Journalism Award – EJAT 2023) katika kundi la Mafuta, Gesi na Madini.

Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo hiyo, Mhe. Nanauka amesema mafanikio ya Esau Ng'umbi ni ushahidi wa uwezo mkubwa wa vijana wa Tanzania wanapopewa nafasi ya kutumia vipaji, maarifa na ubunifu wao katika kujenga taifa. Amesema tuzo hiyo ni heshima si kwa Esau pekee, bali pia kwa sekta ya habari na vijana wote wa Tanzania wanaoendelea kufanya vizuri katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Waziri Nanauka ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuthamini na kuhamasisha vijana wanaofanya kazi kwa bidii na ubunifu, huku akiwataka kutumia mafanikio yao kama chachu ya kuwainua vijana wengine na kuchangia maendeleo ya nchi.

Mbali na kutwaa tuzo katika kundi la Mafuta, Gesi na Madini, Esau Ng'umbi pia ametambuliwa kama mshindi wa pili (Runner-up) katika makundi mengine mawili ya tuzo hizo, jambo linaloonesha kiwango chake cha juu cha weledi, ubora na umahiri katika tasnia ya habari.

Kwa upande wake, Esau Ng'umbi amewashukuru Watanzania wote kwa kuendelea kumuamini na kuunga mkono kazi yake ya uandishi wa habari. Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za muda mrefu, kujifunza kwa kuendelea na ushirikiano alioupata kutoka kwa wadau mbalimbali wa sekta ya habari.

Aidha, amemshukuru Mhe. Joel Arthur Nanauka kwa pongezi na baraka alizompatia, akisema hatua hiyo inaonesha namna Serikali inavyotambua mchango wa vijana katika maendeleo ya taifa. Ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na uzalendo ili kuhabarisha umma na kuchangia maendeleo ya Tanzania.

Tukio hilo limefanyika katika Ofisi Ndogo za Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana zilizopo katika Jengo la Utumishi, jijini Dar es Salaam.