Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
MAFUNZO YA SHERIA ZA UNUNUZI YAFIKIA TAMATI,WAHUDH...

MAFUNZO YA SHERIA ZA UNUNUZI YAFIKIA TAMATI,WAHUDHURIAJI WAAHIDI MAKUBWA.

09 May, 2026
MAFUNZO YA SHERIA ZA UNUNUZI YAFIKIA TAMATI,WAHUDHURIAJI WAAHIDI MAKUBWA.

Na Byarugaba Innocent, Arusha

Mkurugenzi wa Utawala na menejimenti ya Rasilimali watu bi. Edith Semtengu Wizara ya Maendeleo ya Vijana amefunga mafunzo ya utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 na Kanuni zake  GN.Na.518 ya Mwaka 2024 kuelekea utekelezaji za bajeti ya mpya ya Wizara ya Mwaka 2026/2027 yaliyokuwa yakiendelea kwenye Ukumbi wa hazina ndogo Jijini Arusha.

Bi.Semtengu ametoa rai kwa Wakurugenzi,Maafisa bajeti na watumishi wengine kwenda kuyatumia mafunzo hayo muhimu kutekeleza majukumu yao ili kuleta tija kwenye taasisi na Taifa kwa ujumla.

Aidha,bi.Semtengu amemshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Vijana Bi.Jenifa Christian Omolo kwa kuridhia na kuidhinisha fedha kugharamia mafunzo hayo baada ya kupokea Ombi kutoka kwa Mkurugenzi wa Ununuzi ndugu Hamis Ally la uwepo wa haja ya watumishi kukumbushwa kwenye Sheria hiyo ya Ununuzi wa Umma.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wengine, Suleiman Mvunye amesema huu ulikuwa muda muafaka kukumbushwa kwenye Sheria hiyo ukizingatia miezi miwili ijayo Wizara ya Maendeleo ya Vijana inakwenda kuanza kutekeleza bajeti yake ya awali tangu kuanzishwa kwake Mwaka 2025.

Aidha,ametoa rai kwa wahudhuriaji wote kutambua kuwa tayari wamepitishwa kwenye Sheria ya Ununuzi wa Umma hivyo wakati wa utekelezaji wa majukumu Sheria hiyo hiyo itatumika kuwaadhibu watakapo kwenda kinyume hivyo ametoa wito kwenda kutekeleza kwa kutumia Sheria,taratibu, Kanuni na Miongozo inayokubalika.