Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mheshimiwa Joel Arthur Nanauka (Mb), leo amezungumza na vyombo vya habari kuelekea uzinduzi rasmi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026.
Amesema kuwa uzinduzi huo utafanyika tarehe 02 Aprili 2026 katika Viwanja vya Gombani, Wilaya ya Chake Chake, Kusini Pemba, ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Amesisitiza kuwa maandalizi yote yamekamilika, huku vijana walioteuliwa kubeba Mwenge wakiwa tayari kutekeleza jukumu hilo kwa siku 195 kwa uzalendo na weledi.
Mheshimiwa Nanauka ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru ni tunu ya Taifa iliyoasisiwa na waasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, ikiwa ni alama muhimu ya uhai wa Taifa letu. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964, Mwenge huo umeendelea kuhamasisha misingi ya amani, umoja wa kitaifa, haki, usawa na uwajibikaji miongoni mwa wananchi.
Kwa mwaka 2026, amesema kuwa Mbio za Mwenge wa Uhuru zitabeba kauli mbiu isemayo “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo,” ikilenga kuimarisha mshikamano wa kitaifa. Aidha, kupitia mbio hizo, wananchi wataendelea kuelimishwa kuhusu mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, rushwa, dawa za kulevya na malaria.
Katika hatua nyingine, Waziri Nanauka amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ushiriki wa vijana katika shughuli za maendeleo kupitia majukwaa ya vijana katika ngazi za Halmashauri. Majukwaa hayo yatawawezesha vijana kushiriki katika maamuzi ya maendeleo, kupata taarifa za fursa mbalimbali pamoja na kujengewa uwezo wa ujasiriamali na ubunifu.
Ameongeza kuwa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 pia zitaambatana na kutembelea, kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo, ili kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha za umma na kuongeza uwajibikaji.
Akihitimisha, Mheshimiwa Nanauka ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huo muhimu wa kitaifa, na kuendelea kudumisha tunu na falsafa ya Mwenge wa Uhuru iliyoasisiwa mwaka 1961 na waasisi wa Taifa letu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nana...
UN CAREERS LIVESTREAM EVENT 2026 Kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Wahitimu Wapy...
WAZIRI NANAUKA AWEKA MIKAKATI YA KUWAWEZESHA VIJANA NA WANAWAKE KIUCHUMI Seri...
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka ame...
Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana kwa kushirikiana na Restless Development leo...