Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
VIJANA WATAMBULIWE KAMA WADAU MUHIMU WA UCHUMI WA...

VIJANA WATAMBULIWE KAMA WADAU MUHIMU WA UCHUMI WA BULUU

08 Oct, 2026
VIJANA WATAMBULIWE KAMA WADAU MUHIMU WA UCHUMI WA BULUU

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, ametoa wito kwa wadau wa kikanda na kimataifa kuwatambua vijana kama washirika muhimu katika utekelezaji wa mipango ya uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na pwani.

Mhe. Nanauka ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Pembeni wa COP 12 wa Mkataba wa Nairobi wenye kaulimbiu “Vijana kama Kichocheo Kikuu cha Uchumi Endelevu wa Buluu katika Ukanda wa Bahari ya Hindi Magharibi”, akisisitiza kuwa vijana wanapaswa kushirikishwa katika sayansi, ubunifu, ujasiriamali, uongozi wa jamii, pamoja na utawala na utungaji wa sera za bahari.

Amesema fursa za uwekezaji, ajira na ujasiriamali katika uchumi wa buluu zinapaswa kupanuliwa kwa vijana, huku ubunifu na teknolojia vikisaidiwa kubadilika kutoka mawazo kuwa suluhisho zinazotekelezeka. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa jamii za pwani na visiwani katika uhifadhi wa mazingira, uvuvi endelevu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumzia nafasi ya vijana, mwanasayansi kijana wa bahari kutoka Taasisi ya Sayansi za Bahari, Irene Jeremiah Tambikeni, amesema nguvu zaidi inapaswa kuelekezwa katika kuwawezesha vijana na jamii za pwani kuongeza thamani ya shughuli zao na kunufaika zaidi na fursa zinazotokana na uchumi wa buluu.

Naye mdau wa uchumi wa buluu, Eric Elieza, amesema changamoto kubwa kwa vijana ni kukosa nafasi ya kushiriki katika maamuzi yanayohusu uchumi wa buluu na usimamizi wa rasilimali za bahari, akitaka vijana kuungana na Serikali na wadau wengine ili kushiriki katika maamuzi, kuendeleza uvuvi endelevu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.