Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA URATIBU WA MBIO ZA...

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA URATIBU WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2026

19 Oct, 2026
KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA URATIBU WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2026

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imepongeza maandalizi na utekelezaji wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, ikieleza kuridhishwa na uratibu uliofanyika kuanzia uzinduzi hadi kilele cha mbio hizo. Pongezi hizo zimetolewa leo, Oktoba 19, 2026, baada ya Kamati kupokea taarifa ya utekelezaji wa miongozo na taratibu za uratibu wa mbio hizo kutoka Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Mhe. Joel Arthur Nanauka.

Akiwasilisha pongezi kwa niaba ya Kamati, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Rejina Christopher Malima amesema Kamati imeridhishwa na maandalizi yaliyofanyika tangu uzinduzi wa mbio hizo hadi kilele chake akimpongeza  Mhe. Nanauka kwa hotuba yake aliyoitoa kwenye kilele cha mbio hizo Mkoani Rukwa akieleza kuwa imeakisi mshikamano na ushirikiano wa timu katika kutekeleza majukumu ya Ofisi hiyo.

Kwa upande wake, Mhe. Nanauka ameishukuru Kamati kwa michango, ushauri, maelekezo na maboresho ambayo yamekuwa yakitolewa katika kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo, kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Waziri, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Kedmon  Mapana, amesema ujumbe wa Mwenge wa Uhuru 2026 umeendelea kusisitiza falsafa, Misingi na maadili ya mbio hizo, ikiwemo kuhamasisha lishe bora na afya imara, mafunzo ya ufundi stadi, upimaji na ushauri wa afya, mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya, kupambana na malaria pamoja na kukuza uzalendo.

Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 zilizinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, na kuhitimishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Pancras Ndejembi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Katika kipindi hicho, Mwenge ulipita mikoa 31 na Halmashauri 195, ukisafiri kilomita 24,877 na kutembelea miradi 1,337 yenye thamani ya takribani Shilingi Trilioni 2.24 zikiongozwa na  kaulimbiu isemayo: “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa Pamoja kuleta Maendeleo.”