Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
TANZANIA NA DENMARK KUSHIRIKIANA MAENDELEO YA VIJA...

TANZANIA NA DENMARK KUSHIRIKIANA MAENDELEO YA VIJANA, VIONGOZI VIJANA KUIBULIWA.

24 Sep, 2026
TANZANIA NA DENMARK KUSHIRIKIANA MAENDELEO YA VIJANA, VIONGOZI  VIJANA KUIBULIWA.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, amekutana na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Jesper Kammersgaard, kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika uwezeshaji na maendeleo ya vijana.

Kikao hicho kimejikita katika kuangalia maeneo ya ushirikiano yatakayosaidia kupanua wigo wa vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi, kupitia upatikanaji wa ujuzi, fursa na programu zinazowawezesha vijana kuanzisha na kukuza shughuli za uzalishaji katika sekta mbalimbali.

Pande hizo zimekubaliana kushirikiana katika kuimarisha ujuzi, uwezeshaji wa vijana kiuchumi na msaada wa kitaalamu (technical support) kwa ajili ya kuhakikisha uendelevu wa miradi inayotekelezwa na vijana, pamoja na kuangalia namna ya kuunganisha programu mbalimbali za uwezeshaji vijana.

Aidha, wamejadili kuhusu kuanzisha programu za kuibua na kukuza viongozi vijana, pamoja na kuunganisha programu za uwezeshaji katika sekta mbalimbali za uzalishaji, ili vijana waweze kutumia ujuzi, ubunifu na vipaji vyao kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Kammersgaard amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika masuala ya vijana, hususan katika kuwaunganisha vijana na fursa za kiuchumi, mitaji, ujuzi na masoko.