Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
NDG. MWANG’ONDA: VIJANA WASIKILIZWE NA KUWEZESHWA...

NDG. MWANG’ONDA: VIJANA WASIKILIZWE NA KUWEZESHWA KUBADILI CHANGAMOTO KUWA FURSA

17 Sep, 2026
NDG. MWANG’ONDA: VIJANA WASIKILIZWE NA KUWEZESHWA KUBADILI CHANGAMOTO KUWA FURSA

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Ndg. Wazo Michael Mwang’onda, amezindua Jukwaa la Vijana la Wilaya ya Uyui katika Uwanja wa Mkesha wa Mwenge wa Uhuru, Isikizya, mbele ya Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mhe. Upendo Wella.

Akiwasilisha taarifa kuhusu jukwaa hilo, Mhe. Wella amesema limeanzishwa ili kutoa nafasi rasmi kwa vijana kushiriki kikamilifu katika maamuzi, upangaji na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui.

Akizungumza na vijana pamoja na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo, Ndg. Mwang’onda amewataka viongozi kujenga utamaduni wa kukutana na vijana mara kwa mara, kuwasikiliza na kubaini changamoto zinazowakabili ili kuzibadili kuwa fursa za maendeleo ya kiuchumi kupitia mafunzo, ubunifu na programu za uwezeshaji.

Aidha, amemwomba Mhe. Wella kuwa mlezi wa karibu wa vijana hao ili wawe na sehemu ya kuwasilisha hoja, changamoto na maoni yao kuhusu masuala mbalimbali yanayogusa maendeleo na ustawi wao.
“Nikuombe wewe pamoja na viongozi wenzako wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kuwaona vijana wote wa Uyui kuwa ni fursa na wala si changamoto,” amesisitiza Ndg. Mwang’onda.

Kwa upande wake, Afisa Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Consolata Charles, amesema jukwaa hilo lina jumla ya wanachama 428, wakiwamo wanawake 313 na wanaume 115. Amesema vijana hao wamejipanga kujadili na kutafuta fursa katika sekta za kilimo, usafirishaji na viwanda vidogo, kwa kuzingatia mazingira na fursa zilizopo katika Wilaya ya Uyui.