Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
NANAUKA: TEKNOLOJIA NA UWEZESHAJI VIJANA VITUMIKE...

NANAUKA: TEKNOLOJIA NA UWEZESHAJI VIJANA VITUMIKE KUJENGA AMANI

22 Sep, 2026
NANAUKA: TEKNOLOJIA NA UWEZESHAJI VIJANA VITUMIKE KUJENGA AMANI

Uwezeshaji wa vijana na matumizi salama na yenye uwajibikaji ya teknolojia za kidijitali vimetajwa kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha amani na usalama wa Taifa, huku vijana wakitakiwa kutumia fursa za teknolojia kwa tija, kushiriki katika kuzuia migogoro na kuimarisha mshikamano wa jamii.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, leo jijini Arusha alipokuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani, yenye kaulimbiu “Sauti za Kidijitali kwa Ajili ya Amani: Kuwawezesha Vijana kuwa Vinara wa Utulivu na Ustahimilivu.

Amesema, amani ni msingi wa maendeleo na kuwa mazingira ya utulivu yanawawezesha vijana kupata elimu, kufanya kazi, kuanzisha biashara, kutumia vipaji na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.

Mhe. Nanauka amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia yanapaswa kwenda sambamba na uwajibikaji, akieleza kuwa matumizi yasiyozingatia maadili yanaweza kuchochea usambazaji wa taarifa potofu, lugha ya chuki na migawanyiko katika jamii. Hivyo, amewataka vijana kutumia majukwaa ya kidijitali kueneza ujumbe unaojenga matumaini, maelewano na mshikamano.

“Tunapowekeza katika vijana, tunawekeza katika amani. Tunapowawezesha vijana kiuchumi, tunaimarisha matumaini,” amesema Mhe. Nanauka, akisisitiza kuwa vijana wenye elimu, ujuzi na fursa wana nafasi kubwa ya kuwa washirika wa maendeleo na walinzi wa amani katika jamii.

Katika hatua za kuimarisha ushiriki wa vijana katika masuala ya amani na usalama, Mhe. Nanauka amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imefanya utafiti wa kitaifa kwa ajili ya maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Vijana, Amani na Usalama.                                                                                                            
Amesema rasimu ya Mkakati huo pamoja na Mpango wake wa Utekelezaji inalenga kuweka mwelekeo wa kitaifa katika kuwawezesha vijana kushiriki katika kuzuia migogoro, kukuza mazungumzo, kukabiliana na taarifa potofu na kushiriki katika michakato ya maamuzi.

Aidha, amesema zaidi ya vijana 2,000 wamefikiwa kupitia shughuli za elimu na uhamasishaji zilizofanyika Dar es Salaam, Tanga, Moshi na Arusha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa na ushiriki wa vijana katika masuala ya amani, usalama na matumizi yenye uwajibikaji ya teknolojia za kidijitali.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla; Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bi. Susan Ngongi Namondo; pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, viongozi wa dini, asasi za kiraia, sekta binafsi, vyombo vya habari, vijana, wabunifu na watayarishaji wa maudhui ya kidijitali.