Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana
KIJANA MTANZANIA ANG’ARA URUSI, AIBUKA MSHINDI WA...

KIJANA MTANZANIA ANG’ARA URUSI, AIBUKA MSHINDI WA PILI ARTMASTERS OPEN

17 Sep, 2026
KIJANA MTANZANIA ANG’ARA URUSI, AIBUKA MSHINDI WA PILI ARTMASTERS OPEN

Yekaterinburg, Urusi 

Yusuf Ally Suleiman ameiletea Tanzania heshima baada ya kushika nafasi ya pili na kutwaa medali ya fedha katika fainali za Kimataifa za ARTMASTERS OPEN zilizofanyika jijini Yekaterinburg, nchini Urusi.

Yusuf ameshiriki katika mashindano hayo akiwa Camera Operator na kufanikiwa kushika nafasi ya pili kati ya timu 10 zilizoshiriki katika mchuano huo, akionesha uwezo, ubunifu na umahiri wa vijana wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Mhe. Fredrick Kibuta, wamepongeza mafanikio hayo na kuahidi kumuunga mkono Yusuf katika jitihada zake za kuendeleza kipaji na taaluma yake.

Aidha, Mhe. Nanauka amewapongeza vijana wote wa Kitanzania walioshiriki katika Tamasha la Vijana la Kimataifa 2026 nchini Urusi, huku akiwahimiza kuendelea kujituma, kuongeza maarifa na kutumia ipasavyo fursa zinazopatikana kupitia majukwaa ya ndani na ya kimataifa.

Mafanikio ya Yusuf yanaendelea kuwa ishara ya uwezo wa vijana wa Tanzania katika sanaa, ubunifu na taaluma mbalimbali, pamoja na umuhimu wa kuwapa nafasi ya kushiriki katika majukwaa ya kimataifa yanayowawezesha kuonesha vipaji na uwezo wao.